msimu wa burudani Highlands fm 92.7

msimu wa burudani Highlands fm 92.7

Friday, July 19, 2013

WEMA AKAMATWA NA KUPANDISHWA KIZIMBANI TENA...



KUNA kila dalili kwamba mrembo anayetamba kwenye filamu za Kibongo, Wema Isaac Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ au Madam jela inamwita na anatakiwa kufanya maombi ili kukwepa kifungo maishani mwake.

Hali hiyo inafuatia staa huyo kupandishwa kizimbani kwa mara nyingine tena Jumatano iliyopita, pale alipopanda katika Mahakama ya Mwanzo ya Kawe jijini Dar kwa kosa la kumpiga na kumtukana matusi ya nguoni meneja wa hoteli moja iliyopo Kawe Beach jijini Dar, Godluck Kayumbu.

Kabla ya kupandishwa kwa ‘pilato’, staa huyo anayemiliki Kampuni ya Endless Fame alikuwa akisakwa na askari kwa siku kadhaa na kufanikiwa kuwapiga chenga za hapa na pale.

ANASWA AKIFUTURU
Hata hivyo, mbio zake ziliishia ukingoni Julai 16, mwaka huu, alipokamatwa saa mbili usiku akiwa anafuturu na wageni wake nyumbani kwake, Kijitonyama Dar.

MTITI KIDOGO
Askari saba walifika nyumbani kwake wakiwa ndani ya Land Rover ‘difenda’ kwa ajili ya kumkamata, hata hivyo walipata upinzani kidogo kutoka kwa mlinzi wa staa huyo ambaye alikuwa akizuia bosi wake asikamatwe ambapo ilibidi askari hao wakaze msuli na kutuliza mtiti uliokuwa ukitaka kutokea.

WEMA AGEUKA MBOGO, ALALA SELO
Baada askari kumfikia staa huyo, walimtaka kwenda naye kituo cha polisi kwa kutumia difenda walilofika nalo ambapo Wema alipinga na kugeuka mbogo kwa kudai kwamba hawezi kupanda difenda kutokana na hadhi yake.
Pamoja na askari kutaka kumpandisha kwa nguvu, staa huyo alipinga na ikakubaliwa apande gari lake aina ya Audi Q7 huku akiwa chini ya ulinzi wa askari.

Safari ikaishia Kituo cha Polisi cha Kawe ambako staa huyo aliandikisha maelezo na baada ya zoezi hilo akatupwa selo.

WEMA HAUOZI
Kama lilivyo jina lake, wema hauozi, staa huyo alipata dhamana saa 5 za usiku baada ya kudhaminiwa na msanii mwenzake wa filamu, Kajala Masanja.
Kajala aliwahi kutolewa katika mdomo wa jela na Wema siku za nyuma baada ya kukutwa na hatia na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar alipotakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 13 au kwenda jela, Wema alimlipia kiasi hicho cha fedha.

WAPAMBE FULL SHANGWE
Wapambe wa Wema waliokuwa wamejazana nje ya kituo hicho cha polisi, walilipuka kwa shangwe baada ya bosi wao kuchomolewa kutoka selo. Staa huyo aliondoka na gari lake lililokuwa likiendeshwa na meneja wa kampuni yake aitwaye Petit Man.

ATEMBEZWA KWA MIGUU
Julai 17, asubuhi Wema alirudi kituoni hapo na kuwekwa chini ya ulinzi kwa ajili ya kupelekwa mahakamani kusomewa mashitaka yake.
Katika hatua ya kushangaza, staa huyo alitembezwa kwa miguu umbali wa mita 200 kutoka kituo cha polisi hadi Mahakama ya Mwanzo ya Kawe.

APANDISHWA KIZIMBANI
Wema alipandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka yake na Mh. Hakimu, Bernice Ikanda na kudaiwa kufanya vurugu, kushambulia kwa kumpiga makofi na kumtukana Kayumbu.
Mbele ya hakimu, Wema alikana mashitaka na hakimu aliiahirisha kesi hiyo mpaka Julai 31, mwaka huu.

IKO SIKU WEMA ATAFUNGWA GEREZANI
Kumbukumbu kutoka kwenye makabrasha yetu zinaonesha kuwa, mrembo huyo ni mtu wa majanga, mara kwa mara amekuwa akifikishwa polisi na mahakamani kutokana na ugomvi.

ALIVUNJA KIOO CHA GARI LA KANUMBA
Mwaka 2009, Wema alidakwa na Polisi Kituo cha Magomeni na baadaye kupandishwa katika Mahakama ya Kinondoni, Dar kwa Hakimu Emilius Mchalu kwa kosa la kuvunja kioo cha gari la aliyekuwa staa wa filamu za Kibongo, Marehemu Steven Kanumba chenye thamani ya shilingi milioni moja. Hata hivyo, Kanumba aliifuta kesi hiyo.

ALIMTISHIA MAISHA BOB JUNIOR
Kama vile haitoshi, mwaka 2011, Wema huyohuyo alikamatwa na Polisi wa Oysterbay jijini Dar na kufikishwa Mahakama ya Mwanzo, Kinondoni kwa kosa la kumtusi na kumtishia maisha mwanamuziki wa Bongo Fleva, Rahem Nanji ‘Bob Junior’.
Katika kesi hiyo, Hakimu Mariam Masamalo alimtia hatiani Wema kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya shilingi 40,000 ambapo alilipa fedha hizo.

ALIMTUSI REHEMA FABIAN
Aidha, mara baada ya Wema kuachiwa huru mahakamani hapo alikamatwa tena na polisi kwa kile kilichodaiwa kumtusi Miss Kiswahili 2008, Rehema Fabian. Wema alipelekwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar kwa maelezo zaidi.

ALIMTUKANA MSANII
Aidha, Wema amewahi kulala kituo cha Polisi Oysterbay, Dar akiwa na mashoga zake, Kajala na Dida kwa madai ya kumshambulia mwigizaji mmoja wa Bongo, kwenye pati iliyofanyika Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay, Dar. Kesi hiyo iliisha kwa mazungumzo nje ya polisi.

No comments:

Post a Comment