msimu wa burudani Highlands fm 92.7

msimu wa burudani Highlands fm 92.7

Monday, June 10, 2013

Zuku Pay Tv na filamu za ki bongo



WASANII wa filamu za Kiswahili hapa nchini wanazidi kupata nafasi nyingine ya kukuza vipato vyao na kuboresha kazi zao baada ya Kampuni ya Zuku Pay Tv kuanzisha channel mpya kwa ajili ya kuonesha filamu za Kiswahili tu.
Uzinduzi wa channel hiyo umefanyika juzi jijini Arusha na kuhudhuriwa na waigizaji na wakuzaji wa filamu Tanzania kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Arusha katika Hoteli ya Naura.
Akiongea katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Satellite, Mohamedi Jenneby, alisema channel hiyo ipo namba 210 inaitwa Zuku Swahili Movies na itapatikana katika vifurushi vyote vya malipo vya Zuku.
Alisema kuwa uzinduzi wa channel hiyo unakwenda sambamba na kushirikiana na waigizaji katika kusaidiana kuboresha kazi zao ambazo zitakapopitishwa kuonekana katika channel hiyo na wao kuingia mikataba ya malipo zitaonekana katika nchi zaidi ya 30 za Afrika.
Alisema hiyo licha ya kuwasaidia kuongeza kipato chao lakini itakuwa ni changamoto kwao katika kujiendeleza kielimu ili kuwawezesha kufanya kazi zao katika ubora unaokubalika kimataifa, hivyo kupanua wigo wa soko lao kimataifa.
Mohammed pia alionesha matumaini yake na kueleza mkakati wa biashara kwa zaidi ya wateja milioni mia moja katika Kanda ya Afrika Mashariki.
“Kiswahili ni lugha ambayo inawaunganisha wakazi wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Lugha ya Kiswahili itaendeleza jukumu muhimu la kuleta maendeleo ya kanda. Channel ya Zuku Swahili inasherehekea maendeleo yetu na kukuza nje utamaduni wetu kupitia filamu duniani,” alisema Mohamed.
Zuku Kiswahili Channel 210 inaonesha filmau, michezo ya kuigiza, majadiiano na muziki. Channel hii inapatikana katika vifurushi vya Zuku Poa, Zuku Classic na Zuku Premium.
Naye Fadhili Mwasyeba, Meneja Mkuu wa Zuku Tanzania aliwashukuru wazalishaji na watunga filamu ambao wameshirikiana na Zuku kuzindua channel hii.
“Kampuni inaendelea kutafuta filamu bora; nia yetu ni kununua haki za kuonesha filamu hii kwenye jukwaa letu la Zuku Pay TV,” alisema.
Alisema Ili kuhakikisha wanakutana na watunga filamu wote kutakuwa na msafara wa ‘Zuku Caravan’ ambao utatembea kote nchini na kuwahimiza wadau wote kukutana na kufanya biashara nao.
Ziara ya kwanza ya msafara itaanza Arusha Juni 15, na baadaye kutembelea mikoa ya Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Morogoro, Dodoma, Shinyanga, Kagera na Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment