KINACHOONEKANA kwa sasa Bongo ni ugumu wa serikali kupambana na vita dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi baada ya jamii kushindwa kubadilika na kuona ugonjwa huo ni wa kawaida kama ilivyo kukohoa au kichwa kugonga.
Hilo limedhihirika baada ya juzi chanzo chetu cha habari kupasha kwamba, baadhi ya wafanyabiashara na wabunge wameingia ‘kazi’ ya kuwanasa mastaa wa kike Bongo, hasa waigizaji wa filamu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, wafanyabiashara maarufu wa jijini Dar na baadhi ya waheshimiwa wabunge wamekuwa wakiwaibukia mastaa wanapokuwa kambini wakirekodi filamu na kuwahonga fedha nyingi sanjari na kuwanunulia magari ya kifahari ya kutembelea.
Inadaiwa wanachofanya baadhi ya mastaa, hasa wakiwa kambini, hupiga picha chafu wakiamini zina mvuto na kuzitundika BBM kwenye simu zao ambapo wafanyabiashara na wabunge hao wanapoziona huweweseka na kuanza msako wa kuwapata.
Chanzo kilisema: “Zamani mapedeshee ndiyo walikuwa wanaongoza kwa kuwachukua mastaa wa kike kwa kutumia picha za mitandaoni na kwenye magazeti, siku hizi mastaa wenyewe wamewashtukia, hawawataki mapedeshee, wanasema fedha zao ni za msimu.
“Siku hizi mastaa wakiwa kambini hupiga picha za hasarahasara na kuzitupia BBM, wafanyabiashara na wabunge wakiziona wanakimbilia kupanga foleni kwenye mahoteli ambayo mastaa hao wamepiga kambi.”
Aidha, chanzo kikasema kuwa baadhi ya wafanyabiashara huhonga kuanzia shilingi 1,000,000 hadi 5,000,000 kama staa ana jina kubwa.
“Kama staa ana jina kubwa, anaweza kuhongwa kuanzia milioni moja hadi tano, kama ni supastaa kama Wema, Wolper, Odama, Rose Ndauka hawa wanaweza kuhongwa hata magari ya kifahari,”kilisema chanzo hicho.
Chanzo kikasema kuwa, mbaya zaidi wanaume hao wamekuwa wakigoma kufanya mapenzi kwa kutumia kinga (kondom) kwa madai kwamba, hawawezi kuhonga pesa nyingi halafu kitandani wakatumia kondom kwani wanakosa raha.
“Kinachouma zaidi ni kwamba, hao wanaume wakiwachukua mastaa hadi chumbani wanakataa kutumia kondom, madai yao pesa wanazohonga ni ndefu (nyingi) kwa hiyo ni afadhali wafaidi, wanasahau kwamba Ukimwi upo.
“Kwa sababu ya tamaa ya pesa, dada zetu (mastaa) wanashindwa kuwa na msimamo wa kutumia kondom. Anaweza kukataa sana, lakini mheshimiwa anaahidi kumnunulia gari, hapo ndipo masharti yanalegezwa,”kilisema chanzo.
Chanzo kikasema kumekuwa na vilio na kusaga meno kwa baadhi ya mastaa kwani wanaponunuliwa magari, kadi zinakaa kwa wanaume hao, baadaye wanawanyang’anya.
“Mbaya zaidi, wapo mastaa waliwahi kushawishika na kutoa penzi bila kinga kwa ahadi ya kununuliwa gari, waliponunuliwa hawakupewa kadi ya kumiliki, baadaye wakanyang’anywa,” chanzo kilitoboa.
Baadhi ya mastaa waliozungumza na paparazi wetu walikiri kuwepo kwa wanaume wenye tabia hiyo, lakini kila mmoja akasema yeye haijamtokea.
Wolper: “Ni kweli, wapo wanaume wanabembeleza sana kutotumia kondom na kuahidi fedha au gari, lakini kama staa anakubaliana na ombi hilo ni kujiangamiza, Ukimwi unaua. Ila mimi sijawahi kukutana na mwanume wa hivyo, kwanza nilishasema ndani ya gari natembea na kondom.”
Jack wa Chuz: “Wewee, uamuzi wa kufanya hivyo ni wa mtu mwenyewe na umri wangu huu nikubali kufanya mapenzi bila kinga kwa sababu ya gari? Kwani gari kitu gani bwana.”
Nisha: “Mh! Nimewahi kusikia kuna wasanii waliingia kwenye mtego huo na sasa wanajuta maana hawana uhakika na afya zao, kwenda kupima wanaogopa, magari walishanyang’anywa, mimi aku!”
Flora Mvungi: “Mimi siwezi kusema kitu maana nina wangu, kama ni gari au pesa ananipa yeye, pole yao ambao hawajajipanga hadi leo.”
Aidha, chanzo kilisema kuwa, maeneo hatari ya kufanyika kwa michezo hiyo ni hoteli kubwa ambazo wasanii hupiga kambi kwa ajili ya kurekodi filamu.
No comments:
Post a Comment